ELIMU ya kuwapenda na kuwalinda watoto wenye ulemavu imekuwa ikitolewa kwa muda mrefu sasa. Lakini, bado kuna baadhi ya wazazi na walezi nchini, wamekuwa wakiwafungia au kuwaficha ndani watoto wao wenye ulemavu.
Kutokana na hali hiyo, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kujenga uelewa na kuhamasisha jamii kupitia njia mbalimbali ili kuwaona watoto wenye ulemavu ni sawa na watoto wengine, wanaopaswa kupendwa na kulindwa, badala ya kuwatenga.
Moja ya jitihada hizo za kutoa elimu ni matembezi yaliyofanyika Dar es Salaam jana, yaliyoongozwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ambayo yaliandaliwa na Shule za Al Muntazir, yaliyoenda sambamba na maadhimisho ya Siku Maalumu ya Usonji Duniani.
Shule hiyo ilianzisha kitengo cha watoto wenye mahitaji maalumu (AMSEN), baada ya kuona kwamba kuna watoto wengi wenye ulemavu, ambao hukosa fursa ya kwenda shule kutokana na sababu mbalimbali.
Sote tunafahamu kwamba ni kweli watoto wengi wenye ulemavu, wamekuwa wakikumbana na vikwazo vya kielimu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mazingira na mfumo wenyewe wa elimu. Tumeshuhudia katika maeneo tofauti, baadhi ya watoto wenye ulemavu wakikumbana na changamoto ya mifumo ya miundombinu katika baadhi ya shule, ingawa serikali imekuwa ikijitahidi kukabiliana na jambo hilo.
Pia, changamoto nyingine ambayo tumekuwa tukishuhudia ni uelewa mdogo kwa watu wenye ulemavu hasa kwa jamii, wazazi na walezi.
Wapo baadhi ya watu, pia wamekuwa wakihusisha hali hiyo na mila potofu, ikiwemo ushirikiano au laana. Uelewa huo mdogo na kutothamini mambo, yanayowahusu watu wenye ulemavu miongoni mwa wana jamii, yamekuwa yakiathiri upatikanaji wa elimu ya uhakika kwa watoto wenye ulemavu.
Hali hiyo imefanya baadhi ya wazazi na walezi kutokuwa tayari kuwaandikisha watoto wenye ulemavu katika shule na hiyo inatokana na mila na desturi, ambazo zinawabagua watoto wenye ulemavu.
Hivyo bado jitihada zinahitajika zaidi katika kutoa mafunzo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu na elimu jumuishi pamoja na kuwepo utayari wa walimu kufundisha watoto wenye ulemavu.
Pia shule zinazotoa elimu jumuishi, zihakikishe zina sifa stahiki za kufundisha watoto wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kuwepo vifaa vya kufundishia na waalimu wa kutosha.
Hivyo, kuna haja kwa wadau wote wa elimu na wapenda elimu na maendeleo hapa nchini, kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba shule nyingi zaidi, zinatoa elimu jumuishi ili kuhakikisha watoto wengi zaidi na wale wa maeneo ya vijijini, wanainuka kielimu.
Ni vyema pia kila mmoja wetu, akashiriki katika nafasi yake kuhakikisha kwamba watoto wenye ulemavu, wanapatiwa mahitaji yao ya msingi ikiwemo elimu bila vikwazo.
Naamini kwamba watoto hawa wenye ulemavu, wakipendwa na kupewa nafasi ya kupata elimu bora, wanaweza kufanya mambo makubwa na kuepukana na utegemezi.
Mamlaka husika nazo ni vyema zihakikishe kuwa malengo ya kumpatia kila mtoto elimu yanafikiwa, bila kuwaacha nyuma watoto hawa wenye ulemavu. Tunaamini kwamba watoto wote ni sawa, hivyo tusiwabague, bali tuwapende
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni